Chungwa
From Wikipedia, the free encyclopedia
Chungwa ni tunda la mchungwa. Jina la kisayansi ni Citrus aurantium L. var. sinensis L. au Citrus sinensis (L.) Osbeck kwenye familia ya Rutaceae. Tunda lifahamikalo kisayansi kama Citrus sinensis huitwa chungwa tamu ili kulitofautisha na Citrus aurantium, chungwa chungu. Chungwa ni mahulusi kati ya mbalungi-kubwa (Citrus maxima) na mchenza (Citrus reticulata).
Mti wake mdogo utoao maua hufikia urefu wa takribani mita kumi na unaota majani yake yasiyokauka muda wote.
Tunda lenyewe ni la rangi ya kijani likiwa bichi na likiwa limeiva rangi yake huitwa kama jina lake: rangi ya machungwa (hii ni sawa katika lugha za Ulaya na lugha nyingine, kama "orange" kwa Kiingereza). Pamoja na limau, danzi, balungi na ndimu ni mojawapo kati ya matunda chungwa, jamii ya matunda ya citrus. Matunda yote jamii ya jenasi ya citrus, huzaliana. Matunda ya jamii hiyo huonwa kama ya aina ya beri sababu ya kuwa na mbegu nyingi, kuwa laini na nyama nyingi huku yakikua kutoka kwenye ovari moja.
Siku hizi chungwa ndilo tunda linalovunwa zaidi kati ya matunda chungwa na ni kati ya matunda yanayovunwa sana duniani.