Ellen Johnson-Sirleaf
Raisi wa 24 nchini liberia / From Wikipedia, the free encyclopedia
Ellen Johnson-Sirleaf (alizaliwa 29 Oktoba 1938 nchini Liberia) amekuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005. Johnson-Sirleaf ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika mashirika ya kimataifa. Baada ya kumaliza masomo katika chuo kikuu cha Harvard, alifanya kazi katika serikali ya Rais William Tolbert mwaka wa 1970 akiwa ni Waziri wa Fedha.
Johnson amekuwa Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika. Hata hivyo yeye sio mwanamke wa kwanza kuongoza nchi barani Afrika. Malikia Zauditu wa Ethiopia aliongoza nchi yake kwa miaka 13 toka mwaka 1917 hadi 1930. Ruth Perry ni mwanamke wa kwanza Afrika kuwa mkuu wa nchi pale alipokuwa mwenyekiti wa urais wa pamoja wa jamhuri ya Liberia toka mwaka 1996 hadi 1997.
Johnson-Sirleaf alihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela mwaka 1985 baada ya kushutumu utawala wa kijeshi nchini humo katika kampeni zake za kugombea ubunge. Alitumia kifungo hicho kwa muda mfupi kabla ya kuachiliwa na baadaye kukimbilia uhamishoni hadi aliporudi mwaka 1997 akiwa anafanyia kazi Benki ya Dunia na Citibank.
Johnson-Sirleaf alimuunga mkono Charles Taylor wakati wa mapinduzi yake dhidi ya Jenerali Samuel Doe lakini baadaye alikuja kuwa mpinzani wake mkubwa na hata kugombea urais dhidi yake mwaka 1997. Taylor alimwandana na hata kumpeleka mahakamani kwa madai ya kuhusika na hujuma za kihaini.
Uchaguzi wa urais mwaka 2005 ulirudiwa baada wagombea urais kutopata kura za kutosha. Katika raundi ya kwanza Johnson-Sirleaf alikuwa wa pili, wa kwanza alikuwa ni mpinzani wake mkubwa George Weah. Katika raundi ya pili ya uchaguzi, Johnson-Sirleaf alitangazwa kuwa mshindi. Hata hivyo, George Weah amepeleka mashtaka mahakama kuu akidai kuwa uchaguzi haukuwa wa haki.
Mnamo Desemba 2021, James Sirleaf mmoja wa wana wa Ellen Sirleaf alikufa katika makazi yake huko Liberia chini ya hali isiyojulikana.