Mali kwa mali
Mali ndio daraja ya moyo kuvuka / From Wikipedia, the free encyclopedia
Mali kwa mali (kwa Kiingereza: barter) ni biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa bila kutumia hela. [1] Kawaida bidhaa zinazobadilishwa zinatakiwa kuwa na thamani sawa. Umbo tofauti la biashari hii ni kulipa kwa bidhaa, yaani kubadilisha huduma kwa bidhaa.
Mali kwa mali ilikuwa njia ya kawaida ya biashara baina ya jamii tofauti kabla ya kusambaa kwa hela. Katika jamii za kisasa si kawaida, isipokuwa katika mazingira ambapo thamani ya pesa imeshuka mno, yaani hali ya mfumukobei mkali.
Biashara ya mali kwa mali inafaa kama watu wawili ambao wana vitu ambavyo vinahitajiwa na mwingine. Ilitokea hasa katika mazingira ya vijijini ambako mazao mbalimbali na bidhaa zilizotengenezwa na wahunzi au wafinyanzi zinaweza kubadilishwa. Ilikuwa kawaida katika Afrika ya Mashariki wakati wa biashara ya misafara hadi karne ya 19 ambako vitu kutoka nje kama vitambaa, ushanga (gololi za kioo), waya, silaha za moto au pombe kali zilibadilishwa kwa pembe za ndovu au watumwa.[2]
Katika mazingira ya biashara ya kubadilishana vinaweza kutokea vitu kadhaa vinavyofanya kazi kama pesa. Mara nyingi ni mifugo; katika Kenya kwenye mwanzo wa karne ya 20 ilikuwa kawaida kukadiria ng'ombe 1 sawa na kondoo au mbuzi 10; viwango hivyo vilikuwa kawaida hadi miaka ya 1930 hivi, pamoja na ushanga (uliitwa "ukuta" pale) na kombe za kauri kwa manunuzi madogo[3].