Majimbo ya Sudan Kusini
From Wikipedia, the free encyclopedia
Majimbo ya Sudan Kusini ni vitengo vya Jamhuri ya Sudan Kusini yenye madaraka ya kujitawala kulingana na katiba ya nchi. Kila jimbo huwa na bunge na serikali yake inayoongozwa na gavana.
Idadi ya majimbo ni 10. Majimbo hayo yaliundwa kutoka kwa majimbo matatu ya kihistoria ya zamani (ambayo ni pia kanda za kisasa) ya Bahr el Ghazal (kaskazini-magharibi), Equatoria (kusini), na Greater Upper Nile (kaskazini mashariki). Majimbo hayo yamegawanywa zaidi katika wilaya (counties) 79 .
Mnamo Oktoba 2015, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit alitangaza kugawa majimbo hayo 10 kuwa 28. Mwezi Novemba 2015 bunge la Sudan Kusini liliidhinisha kuundwa kwa majimbo mapya. Mnamo Januari 2017, Rais Salva Kiir alitangaza amri ya kuongeza tena idadi ya majimbo kutoka 28 hadi majimbo 32. [1]
Lakini kwenye Februari 2020 nchi ilirejea katika majimbo 10 ya awali pamoja na maeneo mawili ya kiutawala, Pibor na Ruweng, na eneo la hali maalum ya kiutawala la Abyei . [2] [3] Mabadiliko hayo yalikuwa tokeo la makubaliano ya amani yaliyomaliza Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Sudan Kusini,
Eneo la Abyei linachukuliwa kuwa sehemu ya Jamhuri ya Sudan na Jamhuri ya Sudan Kusini kwa wakati mmoja. Eneo la Kafia Kingi linazaniwa kati ya Sudan Kusini na Sudan na Pembetatu ya Ilemi inazaniwa kati ya Sudan Kusini na Kenya.