Mapenzi ya jinsia moja
From Wikipedia, the free encyclopedia
Mapenzi wa jinsia moja (kwa Kiingereza: homosexuality) ni mwelekeo wa kimapenzi kati ya watu wa jinsia ileile. Mwelekeo ukifuatwa unageuka tabia.
Mwelekeo wa kimapenzi humaanisha mihemko ya kimahaba au mivuto ya kimapenzi kwa jinsia fulani. Mwelekeo huo kwa kawaida humfanya mtu kupenda jinsia tofauti na ya kwake (kuwa na mvuto kwa watu wa jinsia nyingine), jambo ambalo linawezesha uzazi kadiri ya maumbile.
Hata hivyo kuna wanawake wanaovutiwa na wanawake wenzao na wanamume wanaovutiwa na wanaume wenzao, mbali ya watu wanaovutiwa na jinsia zote mbili (kwa Kiingereza: “bisexual”), mbali na wale wasio na mwelekeo wowote wala kusikia mvuto wowote wa namna hiyo (kwa Kiingereza: “asexuals”).
Watu wana mang'amuzi tofauti juu ya mwelekeo wao wa kimapenzi. Baadhi wanajitambua kwa muda mrefu kabla hawajaanza uhusiano na wengine. Baadhi hujihusisha na vitendo vya kimapenzi kabla ya kujitambua na kuchukua msimamo juu ya mwelekeo wao. Vivutio vya msingi ambavyo huunda mwelekeo wa kimapenzi wa watu wazima kwa kawaida huibuka katika ubalehe.[1] Wakati huo wengine wanayumba kwa muda fulani katika kujitambua, lakini baadaye wengi wao wanakomaa katika mwelekeo wa kawaida [2]. Wapo wanaotaka hao watoto wapewe mapema dawa za kuzuia ubalehe ili baadaye iwe rahisi kuwafanyia upasuaji wa kubadili vyungo vya uzazi kadiri ya mwelekeo wao kama kwamba mwili ulivyo hauna maana. Serikali za nchi mbalimbali, kama Uswidi, Ujerumani na Uingereza, zimeshatakaza tiba za namna hiyo kwa kuona madhara yake kubwa.
Binadamu, akiwa na akili na utashi, halazimiki wala hapaswi kufuata mielekeo yake yote, bali anatakiwa kuidhibiti, la sivyo ataharibika upande wa afya ya mwili na ya nafsi vilevile, mbali ya kuharibu maisha ya jamii. Kwa mfano, mtu anaweza kuwa na mwelekeo wa kuwazini watoto wadogo, mwingine wa kula kupita kiasi, n.k. Wakifuata mielekeo hiyo ataleta madhara tu. Maadili yanafundisha kufikiri kabla ya kufuata mwelekeo wowote.