Kipindupindu
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kipindupindu (kwa Kilatini na Kiingereza cholera kutoka neno la Kigiriki χολέρα, kholera, lililotokana na χολή, kholē, nyongo) ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba. Bakteria hizo ambazo huitwa vibriocholerae huweza kusababisha kuhara sana na kutapika sana pamoja na homa kali.
Maambukizi hutokea hasa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi. Wadudu hao huweza kuchafua vyakula endapo vyakula hivyo vitaachwa wazi bila kufunikwa na chombo chochote na kuvutia nzi hao kutua juu ya vyakula hivyo na kuacha bakteria zitakazosababisha ugonjwa wa kipindupindu kwa mtu atakayekula chakula kile.
Kiwango cha kuhara na kutapika kinaleta upungufu wa maji na uwiano wa chumvi mwilini. Baada ya dalili hizo kutokea kuna hatari ya kifo kwa asilimia 20 - 70 ya wagonjwa kama hawana tiba.
Tunaweza kujilinda na kipindupindu endapo tukajilinda na vitu vifuatavyo ambavyo ni kunywa maji safi na salama na kula chakula kisichopoa. Bila kusahau kusafisha maeneo yote yanayomzunguka kiumbe hai, hasa binadamu. Yatupasa kufanya usafi katika mikoa yetu yote, hasa majijini ambako kunashutumiwa sana kuwa machafu.