Sirili wa Aleksandria
From Wikipedia, the free encyclopedia
Sirili wa Aleksandria (Theodosios, Misri, 370 hivi - Aleksandria wa Misri, 444) alikuwa Patriarki wa Aleksandria, Misri (kuanzia tarehe 18 Oktoba 412 hadi kifo chake) na mwanateolojia.
Alishiriki mabishano ya karne ya 4 kuhusu imani juu ya Yesu Kristo akitetea dogma ya umoja wa Nafsi yake ya Kimungu kwa kutegemea daima mapokeo ya Kanisa na mamlaka ya mababu waliomtangulia, hasa Atanasi. Kwa ajili hiyo aliitwa “mlinzi wa usahihi” (wa imani).
Mtu wa hamaki na mwenye uwezo wa kufanikisha mambo yoyote, ni maarufu hasa kwa kumkomesha Nestori wa Konstantinopoli katika Mtaguso wa Efeso (431) uliomtangaza Bikira Maria kuwa Mama wa Mungu. Vilevile alikuwa mkali dhidi ya wazushi wengine, Wayahudi na Wapagani, na hata dhidi ya Yohane Krisostomo.
Kwa kweli ulikuwa wakati mgumu ambapo ukweli uliweza kushinda uzushi kutokana tu na wachungaji wenye msimamo mkali katika kulinda kundi la waamini walilokabidhiwa[1].
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1883 Papa Leo XIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.