Virusi vya UKIMWI
From Wikipedia, the free encyclopedia
Virusi vya UKIMWI; kifupi: VVU; kwa Kiingereza HIV, yaani "Human Immunodeficiency Virus") ni virusi vinavyoshambulia mwili wa binadamu kwa kuondoa nguvu zake za kupambana na maambukizi nyemelezi yanayosababisha maradhi.
UKIMWI ni ugonjwa wa mfumo wa kingamwili wa binadamu [1] ambao ni hatari sana katika maisha ya binadamu kwa kuwa husababisha vifo. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kufikia mwaka 2014 ugonjwa huu umeua watu milioni 39, hasa kati ya wanaoishi barani Afrika kusini kwa Sahara. Kwa mwaka 2015 pekee wamefariki watu milioni 1.2 na kati yao watoto wengi.
UKIMWI umekuwa na madhara makubwa katika jamii, kama ugonjwa wa mwili na kama chanzo cha ubaguzi. Kuna sintofahamu kuhusu UKIMWI kama vile kwamba eti, unaweza kusambazwa kwa kugusana tu bila ngono.
Ugonjwa huo pia unasababisha madhara ya kiuchumi ambayo ni makubwa, hasa kwa nchi maskini.
UKIMWI hadi hivi sasa haina chanjo wala tiba, lakini tunaweza kuuepuka ugonjwa huu kwa kuachana na ngono ambayo huweza kusababisha ugonjwa huo, pia tunaweza kujikinga nao kwa kuepuka kuchangia vifaa au vitu vyenye ncha kali.
Kimsingi zaidi ni kwamba ugonjwa huo umetokana na kuenezwa hasa na maadili mabovu. Dhidi yake watu wanahitaji kuelewa tangu utotoni na ujanani maana ya jinsia na maisha kwa jumla, kwamba vinadai upendo, nidhamu na uwajibikaji, si kufuata tamaa tofautitofauti daima[2].
Tarehe 1 Desemba kila mwaka ni siku ya UKIMWI duniani.