Madonda matakatifu
From Wikipedia, the free encyclopedia
Madonda matakatifu (kwa Kilatini na Kiingereza Stigmata, wingi wa stigma, kutoka Kigiriki στίγμα) ni jina linalotumiwa na Wakristo kutaja majeraha au maumivu katika viungo vya mwili ambapo Yesu alipatwa na madonda 5 wakati wa kusulubiwa, yaani mikono, miguu na ubavu, lakini pia kichwa na sehemu nyingine alipotiwa taji la miiba au kupigwa mijeledi.
Mtume Paulo mwishoni mwa Barua kwa Wagalatia aliandika, "Mimi nachukua mwilini mwangu chapa (stigmata) za Yesu."[1] kama zile zinazotiwa juu ya mwili wa wanyama au watumwa ili kutambua ni mali ya nani. Inafikiriwa kwamba alikuwa anadokeza alama za mapigo aliyoyapata kwa ajili ya imani yake.
Watu waliopata alama za namna hiyo lakini bila mapigo ya kawaida walitokea hasa katika watawa wa Kanisa Katoliki kama vile Wadominiko na Wafransisko.[2]
Wa kwanza kujulikana ni shemasi Fransisko wa Asizi. Baada yake kesi hizo ziliongezeka, lakini madonda hayo yanapatikana tu ndani ya wale wanaotoka nje ya nafsi, yakitanguliwa na kuongozana na maumivu makali ya kimwili na ya Kiroho yanayowalinganisha na Yesu msulubiwa.Padri wa kwanza ni Pio wa Pietrelcina.